Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni leo imesaini mkataba na Kampuni mbili za China kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa barabara zenye urefu wa kilomita 12 ambapo jumla ya kiasi cha Tsh. Bil. 34.2 zitatumika kwenye mradi huo.
Kampuni ambazo Manispaa ya Kinondoni imeingia mkataba wa ujenzi huo mara baada ya kutangazwa tenda ni Stecol Corporation pamoja na China Ralway Seventh Group Limited.
Mkataba huo umesainiwa na Mstahiki Meya Mhe. Benjamini Sitta, na kushuhudiwa na Kaimu Mkurugenzi Dk. Patricia Henjewele pamoja na Kaimu Mhandisi wa Manispaa Mkelewe Tungaraza.
Akizungumza mara baada ya hafla ya utiwaji wa saini wa mkataba wa mradi huo, Meya Sitta amefafanua kuwa ujenzi huo utahusisha barabara ya Magomeni mapipa hadi urafiki ambayo inaurefu wa zaidi ya kilomita saba (7), Makumbusho, Mwanamboka, na barabara ya Muhimbili ambazo zinaurefu wa zaidi ya kilomita tano (5).
Aidha Meya Sitta ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Magomeni Mapipa na Urafiki inajengwa na Kampuni ya Stecol Corporation kwa gharama ya Tsh. Bil. 18.7 huku barabara ya Makumbusho, Mwanamboka na Muhimbili ikijengwa na Kampuni ya China Ralway Seventh Group Limited kwa gaharama ya Tsh. Bil.15.5.
Mhe. Sitta amemshukuru Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kwa kuhakikisha barabara hizo zinajengwa na kwamba maendeleo ambayo yanafanyika katika Manispaa hiyo yanatokana na juhudi kubwa ya utendaji kazi wake.
“ Nampongeza Mkurugenzi wetu, anafanya kazi kubwa leo hii tunakwenda kuleta maendeleo makubwa ya barabara katika Manispaa yetu, hivyo mradi huu utakuwa sehemu ya kutatua changamoto zilizopo katika Halmashauri yetu” amesema Meya Sitta.
“ Leo ni siku ya kihistoria katika Manispaa yetu, tumesaini mikataba mikubwa miwili kutoka kampuni mbili tofauti , mikataba hii nisehemu kubwa ya mradi wa DMDP, ambao unakwenda kutatua changamoto ya barabara kwenye Halmashauri yetu , hivyo ninampongeza sana Mkurugenzi wetu Kagurumjuli” amesema Meya Sitta.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa DMDP ambaye pia ni Kaimu Mhandisi wa Manispaa, Mkelewe Tungaraza amesema kuwa mradi huo utaanza Aprili mwaka huu na unatarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi 15.
Imeandaliwa na Kitengo Cha habari na Mahusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.