Manispaa ya Kinondoni imeandaa mafunzo ya siku moja kwa Watendaji wa Kata na Mitaa yenye lengo la kuwawezesha kutekeleza jukumu la msingi la utambuzi wa maeneo pamoja na barabara ili zoezi la anwani za makazi liweze kukamilika kwa wakati na ufanisi.
Akifungua semina hiyo ya siku moja kwa Watendaji hao Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Salum Yusuph amesema Watendaji wa Kata na Mitaa ndio watu muhimu katika kufanikisha azma nzima hasa ikizingatiwa utekelezaji wa majukumu yao unagusa wananchi moja kwa moja.
"Ninyi Watendaji mnaotekeleza majukumu yenu kwenye Kata na Mitaa, huko ndio mnaojua eneo hili ni lipi na barabara hii ni ya wapi, ndio mnaotekeleza majukumu yanayogusa wananchi moja kwa moja, hivyo kwa zoezi hili bila nguvu yenu, uwajibikaji wenu, ufanisi wake utakuwa mgumu. Niwaombe mshiriki uwezeshaji huu wa siku moja kwa ufanisi ili tuweze kwenda sawa kufikia lengo kusudiwa". Amesema Salum Yusuph.
Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo pia amezitaja faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa zoezi zima la anwani za makazi kuwa ni kurahisisha zoezi la sensa linalotarajiwa kuanza mwezi wa nane, litarahisisha upatikanaji wa huduma, litasaidia katika ukuaji wa uchumi, ulinzi na usalama wa mtu binafsi na Taifa, litatoa mwelekeo wa upatikanaji wa fursa mbalimbali na kusaidia utambuzi wa nyumba na idadi ya wakazi wa eneo husika.
Alpokuwa akitambulisha mada zilizoandaliwa kwa Watendaji hao wa Kata na Mitaa, Mwenyekti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule Ndg. Geofrey Mwamsojo amesema mafunzo haya yatarahisisha utekelezaji wa zoezi hili na kuwataka watendaji hao kuzingatia ili waweze kukabiliana na kikwazo chochote katika ukamilishaji wake.
Mada zilizofundishwa ni pamoja na mwongozo wa mfumo wa anwani za makazi, ukusanyaji wa taarifa, manufaa ya mfumo wa anwani, majukumu ya kila mmoja, pamoja na utoaji na upatikanaji wa taarifa.
Mafunzo haya ya siku moja yamehusisha Watendaji wa Kata zote 20 na Mitaa 106.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.