Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya nchini. Hatua hii imekuja baada ya Halmashauri kutenga fedha za kununua magari mawili ya kubeba wagonjwa kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa huduma za dharura za afya kwa wananchi.
Akizungumzia uamuzi huo, Mei 7 2024 alipokuwa katika Kikao Cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kinondoni katika Ukumbi wa Manispaa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Saad Mtambule, alielezea kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya katika ngazi zote.
Alisema, "Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya magari 150 ya kubeba wagonjwa katika vituo mbalimbali vya afya nchini. Mojawapo ya Vituo vya Afya vilivyonufaika ni Kituo Cha Afya Kigogo." Aliongeza kuwa, "Katika kuunga mkono hatua hiyo, Manispaa yetu imetenga fedha kununua magari mawili ya kubeba wagonjwa, ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wananchi kwa kuwafikisha haraka katika vituo vya afya pale wanapohitaji matibabu ya dharura."
Aidha, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Mheshimiwa Songoro Mnyonge, ameahidi ujenzi wa Kituo Cha Afya cha kisasa katika Kata ya Mikocheni ili kuboresha sekta hiyo.
Alisema, "Lazima tufanye kitu ambacho mtu yeyote akija atasema hii ni Kinondoni. Hivyo tunaahidi ujenzi wa Kituo cha Afya cha kisasa katika Kata ya Mikocheni na kitakachokuwa na hadhi ya kubwa kuliko kile kilichopo katika Kata ya Kinondoni."
Kwa ujumla, jitihada za serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini. Katika hilo, Manispaa ya Kinondoni imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya kubeba wagonjwa na ujenzi wa Kituo Cha Afya katika Kata ya Mikocheni ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.