Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeadhimisha siku ya wazee duniani iliyoambatana na kauli mbiu isemayo "Tuimarishe usawa kuelekea maisha ya uzeeni" kwa kutoa huduma za Upimaji afya kwa wazee zaidi ya 200.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo katika viwanja vya mwinjuma vilivyoko katika Kata ya Makumbusho ambapo mgeni rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mh.Benjamin Sitta.
Katika kuadhimisha siku ya wazee, Meya Sitta amesema changamoto kubwa inayowakabili wazee ni changamoto ya afya, hivyo Manispaa imeamua kupima afya za wazee hao na kutoa ushauri wa masuala ya afya kwa wazee ili kuweza kuimarisha afya zao.
Pia ameitaja mikakati iliyowekwa na Manispaa ya kinondoni katika kuimarisha afya za wazee kuwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata kadi za msamaha wa matibabu zitakazowapa uhakika wa matibabu bure katika vituo vyote vya afya na zahanati zote za serikali.
Naye Afisa ustawi wa jamii wa Manispaa hiyo amesema Manispaa katika kuhakikisha inawapatia wazee matibabu bure, Tayari imeshagawa vitambulisho 12,183 vya matibabu bure kwa wazee wa kuanzia umri wa miaka 60 na zoezi hili ni endelevu.
Katika hatua nyingine mwakilishi wa wazee amebainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili kuwa ni pamoja na kukosa baadhi ya dawa katika baadhi ya vituo vya afya, uchache wa vituo vya kulelea wazee wenye mahitaji maalum, posho ya kujikimu ya kila mwezi na kutokuwepo kwa miradi ya wazee ili iweze kuwasaidia kiuchumi.
Huduma za afya zilizotolewa katika maadhimisho hayo ni pamoja na kupima pressure, kisukari, macho, elimu ya lishe, pamoja na kuandikisha kadi za msamaha wa matibabu.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.