Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeadhimisha siku ya wazee duniani iliyoambatana na kauli mbiu isemayo "Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Tuthamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee" kwa kugawa kadi hamsini za msamaha wa matibabu kwa wazee.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo katika viwanja vya mwinjuma vilivyoko katika Kata ya Makumbusho ambapo mgeni rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mh.Benjamin Sitta.
Katika kuadhimisha siku ya wazee, Meya Sitta amesema ipo mikakati madhubuti ambayo imeandaliwa na Manispaa ili kuhakikisha haki zao zinapatikana.
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni utaratibu wa kuwatembelea wazee na kufanya mikutano ili kuwasikiliza, kutoa elimu kwa wazee kuhusu uelewa juu ya umuhimu wa kujisajili ili kutambulika na kupatiwa huduma ya vitambulisho na kuhakikisha wazee wote wenye umri kuanzia miaka 60 wanapata vitambulisho vya msamaha kwa matibabu.
Aidha amewataka wazee kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata maoni yao, kwani ndio njia rahisi ya wao kuweza kutambulika na kupatiwa fursa zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi na kiafya.
"Ni rahisi kudeal na vikundi, ni rahisi kuthamini vikundi, ni rahisi kupata maoni ya vikundi kuliko kuhangaika na mtu mmoja mmoja" alisisitiza Meya.
Naye Afisa ustawi wa jamii wa Manispaa hiyo Bi Khalili Katani ameainisha changamoto zinazojitokeza katika zoezi la utambuzi wa wazee kuwa ni kushindwa kutoa umri wao halisi wa kuzaliwa, kusajili kwa wazee ambao si wakazi wa kudumu wa Wilaya ya Kinondoni, wazee wengi kusumbuliwa na magonjwa sugu na nyemelezi Kama kisukari, kupooza, pumu, Kurukwa na akili, moyo, mgongo, macho, miguu, ganzi, kiuno na magoti.
Katika hatua nyingine muwakilishi wa wazee Bw. Nasoro Mataula katika risala yake ameishukuru Halmashauri kwa kuwapatia kadi za msamaha wa matibabu zitakazorahisisha kushughulikia afya zao.
Madhimisho hayo yameambatana na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili kutoka kwa wapogoro pamoja na zoezi la kufukuza kuku.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.