Kinondoni kwa kushirikiana na shirika la Engender Health Imeadhimisha siku ya watu wenye ulemavu duniani yenye kauli mbiu isemayo "Si kila ulemavu unaonekana", kwa kutoa huduma za afya ya uzazi bure kwa kundi la watu wenye ulemavu.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika kituo kipya cha Afya cha Kigogo ambapo watu wenye ulemavu wamepata huduma mbalimbali za afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi, Ushauri juu ya matumizi ya uzazi wa mpango, masuala ya ukatili wa kijinsia pamoja na huduma nyingine za kiafya.
Akiongea wakati wa maadhimisho hayo, Mratibu wa ubora wa huduma za afya toka Kinondoni, Dkt Zuhura Manyama amesema wameadhimisha siku hii katika kituo cha afya ili kufikisha ujumbe kwa Jamii kuwa walemavu pia wanayo haki ya huduma za afya ya uzazi kama watu wengine na kuwataka wauguzi wa afya kusimamia misingi yao ya kazi inayowataka kutoa huduma sawa kwa wote na si vinginevyo.
"Wenzetu ambao wana ulemavu waelewe kwamba Wana haki sawa na raia wengine wote, wao Kama wananchi wanapata huduma hapa wanastahili kupewa huduma sawasawa na wale wengine, huduma ambazo Zina ubora uleule" Amesisitiza Dkt Zuhura
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Engender Health Bi Prudence Masako amesema shirika lake linashirikiana na Serikali katika kutoa huduma bora za Afya kwa watu wote, hivyo kwa leo wameamua kusaidia huduma za afya kwa kundi la watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yao muhimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa scalling of family planning programs wa Engender Health Dkt Moke Magoma amesema kuwa wenzetu wenye ulemavu ni sehemu ya kipaumbele cha Mradi, hivyo shirika limefarijika kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni kupitia kamati ya uendeshaji wa afya ya Halmashauri kwa kuwapa huduma watu wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine Mratibu wa Umoja wa wanawake viziwi Tanzania ( UWAVITA) Bi Aneth Mdemu ameishukuru Manispaa ya Kinondoni kwa niaba ya wenzie wanaoishi na ulemavu kwa kuwasogezea huduma za afya ya uzazi karibu na jamii yao na pia kwa kupata elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu Afya kupitia wakalimani wa lugha ya alama.
Siku ya watu wenye ulemavu Duniani huadhimishwa kila tarehe 3 mwezi Disemba ambapo , kwa mwaka huu kitaifa yanaadhimishwa Mkoani Dodoma.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.