NI AGIZO LA NAIBU WAZIRI WIZARA YA ARDHI ,NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MH ANGELINA MABULA KATIKA KIKAO KAZI CHAKE NA WATENDAJI WA IDARA YA MIPANGOMIJI, ARDHI NA UTHAMINI MANISPAA YA KINONDONI.
Manispaa ya Kinondoni imetakiwa kuweka mpango mkakati wa kuhakikisha inakusanya madeni yote yatokanayo na kodi ya Ardhi kwa wadaiwa sugu ili fedha hizo ziweze kutumika katika kuendeleza miradi ya Maendeleo.
Agizo hilo limetolewa leo na Naibu Waziri Wizara ya Ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi Mh Angelina Mabula alipokuwa katika kikao kazi chake pamoja na watendaji kutoka Idara ya Mipangomiji, Ardhi na Uthamini kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Amesema ni vema ukawepo utaratibu mzuri wa kuhakikisha madeni na kodi hizi za Ardhi zinakusanywa ili fedha hizo ziweze kutumika katika kutekeleza miradi ya Maendeleo .
"Wekeni Mapango mkakati wa kukusanya madeni, na madiwani hakikisheni mnapokaa kwenye vikao vyenu vya kila robo mmeletewa orodha ya wadaiwa waliopatiwa notisi kwa ajili ya malipo "Amesisitiza waziri .
Aidha amesema kikao kazi chake pamoja na mambo mengine ni kwa lengo la kukagua mfumo wa ukusanyaji mapato katika sekta ya Ardhi, kuangalia utendaji kazi wa mabaraza ya Ardhi pamoja na kuangalia namna ya kuendeleza maeneo yetu kupitia shirika la nyumba (NHC).
Naye katibu Tawala Wilaya Kinondoni Bi Gifti Msuya kwa Niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni katika taarifa yake kwa Naibu Waziri Wizara ya Ardhi amesema idara ya Mipangomiji inazo changamoto ambazo zikifanyiwa kazi watakuwa katika hatua nzuri ya utekelezaji
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni ufinyu wa nafasi katika masijala ya ardhi, matumizi ya mfumo usiokuwa wa kielektroniki katika kutoa huduma, uwepo wa madalali na mwingiliano wa utekelezaji wa majukumu baina ya Wizara na Halmashauri.
Nyingine ni uvamizi wa maeneo, ujenzi holela, ufinyu wa bajeti katika kutoa fidia, wananchi kuwasilisha nyaraka za kughushi pamoja na ukusanyaji kodi maeneo yasiyopimwa.
Katika hatua nyingine Mweyekiti wa baraza la Ardhi la Kinondoni Ndg Yose Mlyambina kwenye taarifa yake kwa Naibu waziri pia ameainisha changamoto za Baraza hilo la Ardhi kuwa ni kuchelewa kwa uteuzi wa wajumbe wa baraza, mfumo wa ulipaji wa ada za Halmashauri kutokuwa rafiki, ukosefu wa miongozo, uelewa mdogo wa sheria na taratibu za mahakama kwa wananchi pamoja na kuwa na mkanganyiko wa amri za utekelezaji kutoka kwa viongozi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutembelea Manispaa ya Kinondoni tangu kuteuliwa kwake kushika nyadhifa hiyo.
Imetolewa
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.