Kufuatia mfululizo wa mvua zinazoendelea kunyesha Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeweka mipango madhubuti katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko hasa ugonjwa wa kipindupindu endapo itatokea.
Hayo yalibainishwa Aprili 12, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mheshimiwa Saad Mtambule katika kikao chake na Watendaji wa Mitaa, Maafisa Afya na Wenyeviti wa Mitaa kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati hiyo.
Akizungumza katuka kikao hicho Mkuu wa Wilaya alisema, "Tujiimarishe kwa kuweka mkazo katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.Tusimamie na tuhamasishe wananchi kufanya usafi, kuondoa taka oza na ngumu ili kurahisisha maji ya mvua kupita kwenye njia yake vizuri bila kikwazo."
Ameongeza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuweka nguvu katika kutokomeza maambikizi. "Viongozi kaeni na Wananchi katika kutoa elimu na hamasa dhidi ya kuacha kutiririsha maji machafu".
Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi. Hanifa Suleiman Hamza amewataka Wenyeviti wasimamie vizuri suala la usafi kwenye maeneo yao kwa kusimamia Sheria za utupaji taka ovyo."Tuonyeshane ushirikiano katika maeneo yetu kwa kuwachukulia hatua kwa wanaotupa taka ovyo na kutiririsha maji ovyo".
Bi. Hanifa ameongeza kuwa, viongozi wahamasishe usafi katika maeneo yao na kutatua changamoto katika maeneo hatarishi.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Ezra Ngereza, alieleza kuwa Kitengo cha Afya kimeandaa mikakati ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu ikiwemo kutoa elimu ya afya kwa wananchi, jamii kupata maji safi na salama. Alisema, "tumeunda timu itakayotembelea nyumba kwa nyumba ili kujua kama kuna maambukizi na kuzuia uuzaji wa vyakula kiholela."
Aidha, Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kinondoni. Bw. Shedrack Maximilian aliwasisitiza Watendaji na Wenyeviti hao kudhibiti uchafu katika maeneo yao.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.