Katika kuongeza mikakati ya kuinua elimu, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, inatarajia kuanza kufundisha wanafunzi kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha kujifunza kwa wepesi zaidi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Hanifa Suleiman Hamza, alipotoa ufafanuzi wa swali la Mheshimiwa Manfred Lyoto, Diwani wa Kata ya Mzimuni.
Diwani huyo alitaka kufahamu mikakati ya uboreshaji elimu ndani ya Manispaa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani lililoketi Agosti 24,2022 katika ukumbi wa Manispaa hiyo.
Mkurugenzi huyo alilielezea Baraza hilo kuwa, ni kweli kuwa siku zote walimu hawatoshi kutokana na kuwa shule na madarasa yamekuwa yakiongezeka kulingana na mahitaji ambapo hata hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuleta walimu.
Alieleza kuwa mkakati wa Manispaa kwa sasa ni kujielekeza kutumia mapato ya ndani kuajiri walimu wa mkataba ili kupunguza nakisi ya walimu.
Aidha alieleza kuwa mwaka jana mwezi Aprili Manispaa ilifanya majaribio ya mfumo wa elimu mtandao ‘visual learning’ kwa kutumia ubao janja ‘smart screen’ katika kufundisha wanafunzi. Kwamba mwalimu atakaa shule moja ambayo itaunganishwa na shule nyingine.
Alilieza Baraza hilo kuwa majaribio hayo yalifanikiwa na kwamba, kwa sasa Manispaa inaendelea kutafuta vifaa vikiwemo ubao janja 'smart screen' zitakazowawezesha wanafunzi kuona kinachofundishwa katika shule nyingine za sekondari haswa katika masomo ya sayansi.
Mkurugenzi aliongeza kuwa ameshatoa maelekezo kwa Afisa Elimu kuandaa bajeti ya kununua smartboards na kuzungumza na watoa huduma za mitandao. “Nishukuru kwamba Afisa Elimu sekondari ametenga kiasi cha shilingi milioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa smartboards ambayo smartboard moja inagharimu shilingi milioni Tano.” Aliongeza kuwa, “kwa sasa mchakato unaendelea wa kumtafuta mzabuni wa kuleta smartboards hizo.”
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mheshimiwa Songoro Mnyonge, aliongeza kuwa, “tunaanza na kiasi hicho cha shilingi Milioni 16, lakini lengo ni kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao ama katika marejeo ya bajeti ya mwaka huu mwezi Desemba, uhitaji ukiwepo tutaongeza fedha ili tuweze kuzitawanya katika shule zetu nyingi za Sekondari”
Aidha, Mkurugenzi huyo pamoja na kueleza kuwa wataendelea kuomba walimu OR-TAMISEMI, pia aliwaomba Waheshimiwa Madiwani hao kuwa kwa vile wao ni wadau wa maendeleo wahakikishe panakuwepo na kumbi za kufundishia wanafunzi hao.
Kikao hicho cha Baraza kimekutana kwa ajili ya kujadili taarifa za robo ya nne (Aprili hadi Juni) ya mwaka wa fedha 2021/2022.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.