Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetoa mkopo zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kwa vikundi 115 vya wajasiriamali ili kuwawezesha wananchi wake kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Mkopo huo umejumuisha vikundi mbalimbali ikiwemo vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni Bi. Stella Msofe wakati akifungua semina ya siku moja ya mafunzo kwa wajasiriamali hao walionufaika na mkopo huo ambao hauna riba.
“Leo tunatoa zaidi ya bilioni 2.5 kwa vikundi 115 vya wajasiriamali kutoka Manispaa ya Kinondoni ikiwa na lengo la kuwakwamua wananchi wetu wa Manispaa hii kiuchumi na kuboresha maisha yao, hivyo tunaomba kila kikundi kurejesha mikopo hii ili na wengine waweze kunufaika na fedha hizi,” amesema Bi. Stella.
Pia Bi. Stella amewataka viongozi wote kutoka Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Manispaa ya Kinondoni kufatilia kwa karibu vikundi hivyo vifanye miradi kama ulivyokusudiwa ili waweze kurejesha mikopo hiyo na wengine waweze kunufaika na fedha hizo ambazo hazina riba.
Lakini pia Bi. Stella amesema kumekuwa na tabia ya vikundi mbalimbali vya wajasiriamali kuchukua fedha za mikopo na kwenda kufanyia mambo mengine ambayo yanawafanya kushindwa kurejesha fedha hizo ili na wengine wanufaike.
“Serikali inapotoa fedha za mikopo sio kwamba ina fedha nyingi hivyo tunawaomba muende kufanya biashara kwa mujibu wa sheria na kanuni zinavyowataka za mkopo huu na sio kwenda kufanya mambo mengine kama kwenda kutunzana kwenye maharusi na mwisho wa siku mnashindwa kurejesha mkopo,” amesema Bi. Stella.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendelo ya Jamii Manispaa ya Kinondoni Bw. Alex Ntiboneka amesema ndani ya mwaka huu walipokea maombi ya vikundi zaidi ya 260 lakini baada ya kufanya tathmini kwa kina wameweza kupata vikundi 115 ambavyo vimeweza kukopesheka.
Mkuu huyo amesema katika vikundi vyote hivyo 115 kuna vikundi wanajishughulisha na ufugaji wa kuku, ng’ombe, usafirisha pamoja na usafi wa mazingira ndani ya Jiji letu la Dar es Salaam.
Lakini pia Bw. Ntiboneka amewaomba wajasiriamali hao waliopewa fedha hizo waende wakafanye biashara kama walivyoandika kwenye andiko la biashra zao wakati wanaomba mikopo hiyo.
Nae Mtahiki Meya Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge ametoa rai kwa vikundi vyote 115 hasa akina mama waache tabia ya kuchukua fedha za mikopo na kwenda kushindana kutoa hela kwenye maharusi na sehemu zingine za sherehe.
“Fedha hizi tunatoa kwa lengo la kuwainua kiuchumi na kuwaboreshea maisha yenu Wanakinondoni hivyo mkiwahi kurejesha inarahisishia wengine waweze kunufaika na fedha hizi,” amesema Bw.Songoro.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.