Akizindua kikao kazi hicho chenye lengo la kujenga uelewa kuhusu mpango wa TASAF wa kunusuru Kaya masikini kipindi cha pili, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe amesema ni vema wakawa na uelewa wa kutosha hali itakayopelekea uwajibikaji utakaoenda sambamba na ufuatiliaji kwa maslahi mapana ya walengwa na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imelenga kuinua kipato kwa kaya masikini hali itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Aidha amewataka viongozi kutambua umuhimu wa mpango wa TASAF kipindi cha pili na kuwataka agenda ya utambuzi wa walengwa kuwa endelevu kwani ndio msingi mzima wa ukamilishaji wa mkakati huu wa kunusuru Kaya masikini kwa maslahi mapana ya Taifa.
"Ningependa eneo hili la upatikanaji wa walengwa kuwe na uwazi wa kutosha kutokana na miongozo ambayo mtaitoa katika mafunzo yenu, ili kwamba tukubali sisi Kinondoni vile vikao vya kisheria na kikatiba tunaiweka agenda hiyo kuwa endelevu", Ameeleza Mhe. Godwin Gondwe.
Ameainisha vipaumbele vinavyotakiwa kutiliwa mkazo katika mpango huu wa kipindi cha pili kuwa ni kuwe na uwazi wa kutosha, kuwe na uelewa mzima wa madhumuni ya TASAF kwa walengwa, tuelewe ni nini wajibu wa walengwa wenyewe na kuhakikisha fedha zinafika kwa walengwa na kutumika kwa malengo mahususi.
Naye Mkurugenzi wa miradi ya jamii TASAF kwa niaba ya Mkurugenzi wa TASAF makao makuu Bi. Philippine Mmary katika hotuba yake amesema katika kipindi cha pili cha TASAF kimelenga kufikia Kaya zote ambazo hazikufikiwa awamu ya kwanza katika Manispaa ya Kinondoni.
Hafla hii ya uzinduzi wa kikao kazi imehudhuriwa pia na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, Mstahiki Meya Kinondoni, Naibu Meya, Baraza la Madiwani, TAKUKURU, Mbunge viti maalum, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Maafisa Ugani kutoka kwenye Kata.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.