Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Stella Msofe leo Jumatatu, Novemba 21, amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla katika uzinduzi wa zoezi la utoaji wa dawa za minyoo, matende na mabusha kimkoa lililofanyika katika shule ya msingi Tandale, Kata ya Tandale Wilaya ya Kinondoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, aliwataka wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kushiriki kikamilifu ili kufikia lengo la kuwezesha walengwa wote wenye umri wa miaka mitano na kuendelea kupata dawa za kudhibiti madhara ya magonjwa hayo kwa kushirikiana na watoa huduma na viongozi wa Serikali za mitaa kama yalivyofanikishwa mazoezi mengine zikiwemo chanjo mbalimbali zilizofanyika kwa nyakati tofauti kwa mafanikio.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuondokana na fikra na dhana potofu zinazoenezwa na Watu wasio na nia njema kuwa dawa hizo zina madhara kwani hazina ukweli na zimethibitishwa kitaalamu kuwa ni salama.
Alisisitiza kuwa hakuna Serikali ambayo inawapenda watu wake kama ya Tanzania inayoweza kuwaletea wananchi wake kitu chenye madhara badala yake inapambana kuwaletea tiba kinga ya kupunguza au kuondoa madhara ya magonjwa haya hususani katika Wilaya za Kinondoni na Temeke zilizothibitika kuwa na maambukizi makubwa katika mkoa wa Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo wataalam wa Afya walianza kwa kutoa maelezo ya vigezo vya ugawaji wa dawa hizo kwa kuzingatia umri, kimo na uzito kisha kutoa dawa kwa kuzingatia vigezo hivyo.
Waliohudhuria katika uzinduzi huo na kunywa dawa hizo ni pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Stella Msofe ambaye alikuwa mgeni rasmi, mwakilishi wa Wizara ya Afya kutoka Makao Makuu Dodoma, mwakilishi kutoka TAMISEMI, Mganga Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Wilaya, wawakilishi wa dini, Walimu, wanafunzi , Wakazi wa Tandale na Wadau wengine wa Afya katika Mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo wawakilishi kutoka MDH.
Wakizungumza katika ugawaji wa dawa hizo za kinga Tiba wote walisisitiza kuwa kuwa dawa hizo zimethibitishwa kitaalam kuwa ni salama na hazina madhara na kwamba wasioruhusiwa kutumia ni watoto chini ya umri wa miaka mitano na wajawazito.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
HALMASHAURI YA MANISPAA YA KINONDONI.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.