Kamati ya kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Kinondoni (CMAC) chini ya mwenyekiti wake ambae pia ni naibu Meya wa Manispaa hiyo Mhe. George Manyama imebaini kuwepo kwa utoro wa walengwa wa dawa za kufubaza VVU, hali ambayo inahatarisha usalama wa afya za wagonjwa hao.
Hayo yamebainika leo wakati wa ziara ya kutembelea vituo vya kutolea huduma kwa Watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi ( CTC) , vilivyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na kituo Cha afya Tandale kwa lengo la kuona hali halisi ya utoaji wa huduma, upatikanaji wa huduma kwa WAVU pamoja na Changamoto.
Akizungumnzia swala hilo la utoro, Mh.Manyama amesema " Hali hii inatishia mapambano yanayoendelea ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI, hivyo ni lazima kwa watoa huduma na wadau mbalimbali tushirikiane na serikali Katika kuongeza juhudi za utoaji wa elimu kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ili waelewe umuhimu wa kuhudhuria cliniki kikamilifu".
Awali akitoa taarifa yake mbele ya kamati, Mkuu wa kitengo Cha Watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Katika hospitali ya mwananyamala Dkt Rehema Mzalau amesema, kwa kipindi Cha mwaka mmoja uliopita idadi ya wagonjwa watoro ni 400, na kubainisha mikakati itakayowawezesha kupatikana kwa wagonjwa hao ili kuzuia uwezekano wa kuambukiza wengine.
Dkt Rehema pia, ameainisha mafanikio yaliyopo kwenye kituo hiko hadi sasa kuwa ni kufanikiwa kupunguza ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto (PPMCTC) Kwani kwa kipindi Cha Mwaka mmoja uliopita kituo kimepata maambukizi 0.
Kwa upande wake mratibu wa Kudhibiti maambukizi ya UKIMWI Manispaa ya Kinondoni Bi Rhobi Gwesso amewasihi wanakamati kuwa sehemu ya uwakilishi katika kutoa elimu kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI juu ya umuhimu wa kuendelea kutumia dawa za VVU, kwani dawa hizi zinafubaza virusi na si kuua virusi.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.