Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo na diwani wa Kata ya Bunju Mhe. Kheri Misinga imetembelea Asasi ya "YCR" pamoja na "LHRO" kwa lengo la kujiridhisha na utekelezaji wa shughuli zihusuzo mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa vijana pamoja na VVU na UKIMWI, lakini pia kujiridhisha na njia zitumiwazo katika kufikisha elimu na ujumbe sahihi kwa walengwa.
Mhe. Misinga amesema dhana nzima ya ziara hiyo pia ni kuweka msingi imara na mpango mkakati wa jinsi ya kushirikiana kwa pamoja na Asasi za kiraia katika kuhakikisha Afua za VVU na UKIMWI pamoja na mapambano dhidi ya dawa za kulevya zinatekelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa hali itakayoleta tija kwa Taifa letu.
"Asasi za kiraia ni wadau muhimu sana katika Halmashauri yetu, kwani tunashirikiana nao kwa karibu sana katika kuhakikisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, pamoja na dawa za kulevya yanafanyika kwa kiasi kikubwa. Wenzetu hawa wanazo njia tofauti za kuwafikia walengwa kwa ukaribu, hivyo tuendelee kushirikiana nao, nisisitize pia tunapotoa elimu juu ya VVU na UKIMWI pamoja na madawa ya kulevya tukumbuke na hili janga la UVIKO-19," Amesema Misinga.
Alipokuwa akijibu suala la UVIKO-19, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Ndg. Samweli Laizer amesema kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 unaoratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Kinondoni imejipanga kutekeleza shughuli hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lengo likiwa ni kufikia wananchi wengi kwa wakati sahihi.
Aidha Dkt. Laizer amesema kuwa ni vema kupata chanjo ya UVIKO-19, kwa hiari kwani ni bora kuliko tiba na kuwataka wananchi kuondokana na dhana potofu zihusianazo na ugumba kwa wanawake na nguvu za kiume.
Naye Mratibu wa kudhibiti UKIMWI Manispaa ya Kinondoni Bi. Rhobi Gweso alipokuwa akizungumza amesema, Kinondoni imekuwa ikishirikiana na Asasi hizi kwa ukaribu sana lengo likiwa ni kusaidiana kwa pamoja kufikia lengo tarajiwa la kupunguza maambukizi katika jamii.
Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Wakuu wa Idara na Vitengo, wawakilishi wa makundi ya dini, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.