Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepongezwa kwa ubunifu wa bidhaa zenye tija hasa katika ushindani wa kibiashara na uuzaji wa bidhaa hizo.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 03/08/2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule wakati akitembelea banda la Manispaa ya Kinondoni katika maonesho ya wakulima (Nane Nane) yanayoendelea mkoani Morogoro mapema leo hii.
"Maonesho ya mwaka huu yamekua tofauti na miaka mingine kwani kumekuwa na ubunifu wa hali ya juu, wadau wamejiandaa vizuri na wana ufahamu wa kutosha kuhusu bidhaa zao na wamekuwa na ubunifu," amesema Mhe. Mtambule.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo amesema, wadau waendelee kuongeza ubunifu ili kuongeza thamani ya bidhaa kwa lengo la kuongeza kupanua masoko, kuongeza uzalishaji, kuondoa tatizo la chakula na kuongeza fursa za ajira.
Mhe. Mtambule amesema maonesho hayo yametoa elimu ya kwamba fursa moja inaweza zalisha fursa nyingine kwa kutolea mfano ufugaji wa mbuzi wa maziwa na ufugaji wa ng'ombe wa maziwa ambao unazalisha maziwa, bidhaa za maziwa (sabuni), gesi ya kupikia kupitia mbolea na ajira kupitia ufugaji huo.
Vile vile, Mhe. Mtambule amesisitiza kuwa Kinondoni iwe na maonesho endelevu ili kukuza teknolojia na kutoa elimu kuhusiana na kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kauli mbiu ya maonesho ya Nane Nane 2023 ni "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula".
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.