NI AGIZO LAKE NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS MAZINGIRA MH. KANGI LUGOLA KUFUATIA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI ZINAZOSABABISHWA NA NCHI ZILIZOENDELEA KUCHAFUA ANGA HEWA.
Halmashauri zote nchini zimetakiwa kuhakikisha zinasalimisha watanzania kwa kushiriki operesheni maalumu ya kusafisha mitaro na kuondoa takataka kwenye kingo za mito iitwayo "TUDHIBITI UCHAFUZI WA MAZINGIRA TUSALIMIKE " inayotarajia kuanza tarehe 01/11/2017, ili waweze kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Agizo hilo limetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Raisi Mazingira Mh Kangi Lugola alipokuwa katika ziara yake kutembelea maeneo yaliyoathirika na mvua ambapo leo alikuwa Tandale kwa Mtogole.
Amesema kampeni hiyo itadumu kwa muda wa miezi miwili na itazinduliwa kwa kufanya usafi kwenye kingo za mito, madaraja na pembezoni mwa barabara ili tuweze kukabiliana na athari hizi zinazopelekea maji kuongezeka na kuathiri kingo za bahari.
"Tanzania yetu hii tunayoifahamu kwa muda sasa tumeanza kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, athari hizi zinasababishwa na nchi zilizoendelea wanavyochafua anga hewa, na matokeo yake sasa tunaanza kupata athari hizi "Amesema Naibu Waziri
Ameongeza kuwa uzinduzi huo utafanyika eneo la mtogole Kwa kuwa ni eneo ambalo linakumbwa na athari za mafuriko, kutokana na uchafu wa Mazingira pamoja na miundombinu ya barabara na mito kutokuwa rafiki.
"Sasa juzi ile mafuriko mliyoyaona ambayo yamesababisha baadhi ya miundombinu, mabarabara madaraja kuharibika makazi ya watu kuingia mafuriko, kupoteza maisha ya watu pamoja na mali zenu ,ndilo chimbuko la kuanzisha operesheni hii "Amesisitiza Naibu Waziri.
Ameongeza kuwa ni chimbuko kutokana na kuwepo kwa mrundikano wa taka ngumu kama vile plastic, matambara na chupa za maji ambazo kwa asilimia tisini zimezalishwa na wanadamu.
Naye Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Ndg Joseph Malongo ameahidi kutekeleza agizo hilo la Naibu Waziri kwa kuwapatia wakurugenzi wa Halmashauri zote waraka utakaotoa mwongozo na maelekezo ya utekelezaji wa agizo la operesheni hiyo .
Kwa nyakati tofauti Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndg Aron Kagurumjuli alipotakiwa kuzungumnzia changamoto za kutozolewa takataka kwa wakati kwenye Halmashauri yake amesema Manispaa inao utaratibu wa kuzoa taka kwenye maeneo ya Umma kama vile kwenye masoko, na kwenye mitaa wanao utaratibu unaoeleweka kabisa wa kuchangisha fedha kwa utaratibu na zinapotimia kutafuta mkandarasi wa kuzoa taka kwa kumsimamia wenyewe.
"Kila mtaa unapaswa kukodi mkandarasi atakayebeba takataka kutoka kwenye mtaa wake, kutokana na fedha walizochangisha, kwa hiyo sio Manispaa kuja kuzoa taka hapana, wao wenyewe kwenye Mitaa wanachangishana fedha kwa mujibu wa utaratibu, hii inafanyika Manispaa nzima lakini pia Manispaa kama Manispaa inawajibika kwenda kuzoa takataka kwenye maeneo ya Umma kama masoko "Amefafanua Kagurumjuli.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri amewataka wananchi kuwa na tabia ya kuzikusanya taka na kuzitupa kwenye maeneo sahihi kama madampo na sio kuzitupa kwenye kingo za mifereji, mitaro ya maji pamoja na pembezoni mwa barabara.
Operesheni hii Maalum yenye kauli mbiu isemayo "Tudhibiti uchafuzi wa Mazingira tusalimike "itadumu kwa miezi miwili kuanzia tarehe 01/11/2017
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.