Green House ni kilimo bora na sahihi katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa mjini.
Hayo yamebainishwa na Bw. John Malecela mmoja wa wakulima anayejishughulisha na kilimo cha mazao ya viungo ikiwemo karoti, nyanya, vitunguu na giligilani kwa kutumia teknolojia mpya ya Kilimo Mjini.
"Nimeamua kujihusisha na kilimo kinachotumia teknolojia mpya baada ya kugundua mazao ya viungo yana umuhimu katika kuleta ladha kwenye vyakula mbalimbali", amesema John.
Aidha, Bw. John amesema kuwa uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na uhitaji wa wanunuzi.
Bw. John ameongeza kuwa kafaidika na maonesho ya wakulima kwa kujifunza kuhusiana na teknolojia ya umwagiliaji wa matone, matumizi sahihi ya mbolea ya mboji na utumiaji wa dawa za asili.
Ameelezea ushiriki wake kwenye maonesho ya Nane Nane yalivyomsaidia kupata fursa ikiwemo elimu kuhusiana na teknolojia mpya ya kilimo pasipo kutumia udongo, namna bora ya utumiaji wa dawa zinazohusiana na na kuua wadudu au kukinga mmea usiathirike (viwatilifu) na kupata masoko.
Vilevile, elimu ya kilimo bila kutumia udongo imekuwa kivutio kwa wadau wengi katika banda la Manispaa ya Kinondoni ambapo Bw. Evody Godrian anaelezea kuwa huzalisha mimea ya salad nyekundu na kijani ambayo soko lake kubwa ni katika Hotel na Supermarket.
"Kilimo hiki masoko yake ni mazuri kikubwa ni elimu iendelee kutolewa ili jamii ijue umuhimu wa matumizi ya salad kwenye jamii kwani wateja wengi sio Watanzania", amesema Evody.
Maonesho ya Nane Nane yamekuwa na faida kubwa kwa kupata wadau wanaohitaji elimu ya jinsi ya kuendesha Kilimo Mjini na hii itapelekea kukua kwa sekta ya kilimo.
Kauli mbiu ya maonesho haya ni "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula".
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.