Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi Hanifa Suleiman Hamza, ameiomba benki ya NMB kuendelea kutoa misaada kwa Manispaa ikiwa ni sehemu ya urejeshaji faida kwa jamii.
Bi. Hanifa ameyasema hayo wakati wa ziara ya Mameneja wa Matawi, Mameneja Mauzo na Afisa Uhusiano wa NMB waliotembelea Manispaa. Uongozi huo wa NMB ulioongozwa na Bi. Mary Marungi ambaye ni Meneja wa Benki hiyo tawi la Magomeni, ulifika kwa ajili ya kutoa shukrani kwa Manispaa ikiwa ni mdau wake wa muda mrefu, kuendelea uhusiano na kumpa pongezi Bi. Hanifa kwa kuendelea kuchaguliwa kuiongoza Manispaa.
"Hivi karibuni tumefanikiwa kujenga vyumba vingi vya madarasa. Hata hivyo, tuna changamoto kubwa ya upungufu wa madawati. Nitafurahi sana iwapo NMB mtatupatia madawati 1,500 kabla ya Desemba mwaka huu," alisema.
Aidha, benki hiyo imeshauriwa kutembelea jengo la Manispaa lililopo Mwenge kwa ajili ya uwekaji matangazo ya biashara.
Naye Mchumi wa Manispaa Bw. Jabiri Chilumba ameishauri benki hiyo kuwa na madarasa ya mfano ya kufundishia kupitia TEHAMA.
"Ni vizuri mkawa na theater za mfano za kufundishia angalau katika shule zetu za msingi na sekondari. Hii, itachangia kuongeza soko kwenu," alisema.
Kwa upande wao, uongozi wa benki hiyo umeahidi kushughulikia maombi ya Manispaa pamoja na changamoto zilizowasilishwa. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.