NI KWA LENGO LA KUSIKILIZA CHANGAMOTO, PAMOJA NA KUWAUNGANISHA NA FURSA MBALIMBALI ZILIZOKO ILI WAWEZE KUJIKWAMUA KIUCHUMI.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi leo, amekutana na wajasiriamali zaidi ya 2000 kutoka katika kata zote ishirini zilizoko Wilayani kwake kwa lengo la kuzungumnzia changamoto pamoja na kuwaunganisha na fursa mbalimbali zilizoko ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mkutano huo uliombatana na kauli mbiu isemayo "Uthubutu, ubunifu na kujiamini "umefanyika katika ukumbi wa King Solomon ambapo wajasiriamali walioshiriki wamepata fursa ya kuzungumnzia changamoto zinazowakabili na kupatiwa mbinu za kujikwamua na changamoto hizo.
Amesema lengo la Halmashauri ni kuhakikisha inaungana na wajasiriamali katika kuhakikisha wanasukuma gurudumu la maendeleo kwa kuwakopesha wananchi wake zana za kufanyia shughuli zao, na hii ni katika kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano inayosisitiza Tanzania ya viwanda.
Aidha amewataka wajasiriamali katika kutekeleza sera ya mikopo ya vijana na wanawake, kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi na kujisajili ili waweze kupatiwa elimu pamoja na fursa mbalimbali za Maendeleo.
Akitoa taarifa ya Mikopo kwa Manispaa ya Kinondoni, Bi Flora Msilu ambaye ni mratibu wa mfuko wa wanawake na Vijana Manispaa hiyo amesema hadi kufika leo, kiasi cha shilingi milioni miambili (200) zimeshatolewa ambapo vikundi 154 zimenufaika na mkopo huo, kati yake 45 ni vikundi vya vijana.
Amezitaja shughuli nyingine wanazojishughulisha nazo katika idara yake kuwa ni kuratibu mikopo, kuhamasisha jamii kupambana na ukali wa virusi vya UKIMWI, Kunusuru kaya maskini kwa kuzipatia fedha ili ziweze kumudu gharama au mahitaji ya msingi (TASAF), ushirikishwaji wa wanawake pamoja na kuratibu maswala ya maafa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatumia taaluma zao kuwasaidia wananchi pale inapohitajika na si vinginevyo.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.