Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi ameonesha kufurahishwa na mabadiliko ya utendaji kazi na utoaji wa huduma unaoendelea hivi sasa katika hospital ya Mwananyamala.
Hayo yamedhihirika leo alipokuwa akitembelea katika wodi mbalimabli za hospital hiyo na kujionea jinsi huduma zinavyotolewa pamoja na mazingira ya usafi yaliyoko hospitalini hapo.
Amesema Hospital ya Mwananyamala imepiga hatua kubwa katika maswala ya utoaji huduma kwa wagonjwa kitu ambacho hakikuwepo hapo awali.
"Aliyoyasema Mh. Diwani kwamba kunamabadiliko makubwa ni jambo la kweli kabisa, mimi binafsi nakiri kwamba mmepiga hatua kubwa Sana Katika namna mnavyowahudumia wananchi, katika namna mnavyotenda kazi zenu, ubora wa zile huduma umeimarika sana "alikiri Hapi.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Festo Dugange alipokuwa akizungumnzia mikakati waliyojiwekea ya kuipandisha hadhi hospitali hiyo amesema kila mwaka wa fedha hutenga bajeti kwenye mpango kabambe wa afya lakini pia mpango wa hospital katika kuboresha Majengo.
Ameongeza kuwa hospital hiyo hutumia mfumo wa mashine katika malipo yake yote na pia swala la nidhamu ndio kipaumbele kikubwa kinachozingatiwa kupelekea makusanyo ya mapato kwa huduma ya NHIF kupanda kwani kila mtumishi huwajibika kwenye nafasi yake, pamoja na kupeana mafunzo na miongozo ya ujazaji wa fomu hizo za NHIF.
Akizitaja faida za mfumo huo Mganga mfawidhi wa Hospital ya mwananyamala Dr. Daniel Nkungu amesema unasaidia kujua idadi ya wagonjwa waliotibiwa, mapato yanayolingana na idadi ya wagonjwa kwa kila kitengo, na kwa kuwa mfumo huu umeunganishwa na bank ya NMB umewarahisishia wagonjwa kuweza kulipia huduma kupitia M. PESA, NMB Mobile, na pia uwezo wa kufuatilia matumizi ya dawa.
Katika hatua nyingine Mganga huyo mfawidhi aliainisha changamoto za mfumo kuwa ni kutopatikana kwa mfumo kwa kiwango kinachotakiwa, na watumiaji pia kutokuwa rafiki nao.
Aidha amezitaja changamoto za jumla za hospitalini hapo kuwa ni uchakavu wa Majengo ,upungufu wa watumishi, mfumo wa majitaka kutokuwa rafiki, kutokuwa na mashine pamoja na sehemu ya kufulia na upotevu wa mashuka ya hospital.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.