NI ENEO LENYE EKARI 4.9 LILILOKUWA DAMPO YA ZAMANI LITAKALOJENGWA SOKO LA KISASA KWA AJILI YA WAFANYABIASHARA WA SOKO LA MABIBO KUHAMIA NA KUFANYA BIASHARA ZAO.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Alli Hapi ametoa mifuko 100 ya cement na Bati 50 kwa ajili ya ujenzi wa choo eneo la kigogo kitakachotumiwa na wafanyabiashara watakaohamia kutoka mabibo na kufanya biashara zao katika eneo hilo.
Ahadi hiyo ameitoa Leo alipokuwa katika mkutano wa hadhara kati yake na wafanyabisahara wa mabibo pamoja na kigogo uliofanyika katika eneo la iliyokuwa kigogo Dampo Manispaa ya Kinondoni.
Amesema eneo hilo kuwa soko ni kufuatia maombi ya wafanyabiashara wa soko la mabibo kuomba kupatiwa eneo la kufanya biashara baada ya kupata changamoto ya eneo walilokuwepo awali.
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuleta Maendeleo na kwa kugeuza eneo hilo kuwa soko ni fursa itakayoleta neema si tu kwa wananchi wa kata ya kigogo, bali kwa wananchi wa Wilaya ya Kinondoni.
"Tumepokea maombi ya wafanyabiashara wa soko la mabibo, kutaka kufanya biashara eneo la kigogo , maombi yenu tumeyapokea, na kwasababu sisi tunafanya kazi kwa niaba ya Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli, tunaendeleza falsafa yake ya kuwaletea wanachi maendeleo, tumeyakubali maombi yenu ya kufanya biashara eneo la kigogo. "Amebainisha Hapi.
Naye Diwani wa kata hiyo, ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mh. Manyama Mangalu amesema fursa hiyo ni ya neema katika kata yake na Manispaa kwa ujumla, kwani pamoja na kufanya biashara itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi kwa wakazi wake wa kigogo pamoja na kuiingizia Halmashauri Mapato.
Katika hatua nyingine DC Hapi ameitaka Manispaa hiyo kuanza kuweka mpango mkakati wa kuboresha eneo hilo kwa misingi ya kuwa soko la kisasa, ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka.
Aidha ameitaka Manispaa kuhakikisha kazi ya mpango wa kujenga choo inaanza mara moja ikienda sambamba na ujenzi wa kibanda cha mlinzi.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano na Habari.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.