NI MGOGORO UNAOHUSU WANANCHI ZAIDI YA 3200
MGOGORO HUUUMEDUMU KWA TAKRIBANI MIAKA 13.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ally Hapi leo amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa maeneo ya Nakasangwe, Nakalekwa na kuwapa ujumbe kuwa mgogoro wa ardhi uliodumu eneo hilo kwa takriban miaka 13 sasa suluhu yake imepatikana.
Hapi ameyasema hayo ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi Wilayani Kinondoni ambapo ofisi yake ilizikutanisha pande mbili za wenye mashamba na wakazi ambazo kwa miaka kadhaa zimekua kwenye mgogoro mkubwa na kufanya nao mazungumzo yaliyoweka msingi mzuri wa kumaliza mgogoro huo.
Aidha Mh. Hapi amewahakikishia wananchi hao kutokuwa na wasiwasi na kwamba serikali Wilayani Kinondoni imeamua kutumia falsafa ya
"Pata kidogo poteza kidogo" (win win solution), ili kumaliza mgogoro huo baina ya pande mbili na kurejesha hali ya amani katika eneo hilo.
"Tumeamua sasa eneo hili lote lipimwe viwanja, ili wakazi wote mliohakikiwa kila mmoja apate kipande cha ardhi cha kuishi na familia yake na viwanja vinavyobaki wapate wenye mashamba. Hii ndiyo njia pekee ya kuweza kuwafanya muishi kwa amani katika mji uliopimwa na kupangwa vizuri."
Alisema DC Hapi
Hali kadhalika, Hapi aliwaeleza wananchi hao kuwa katika eneo hilo zaidi ya viwanja 6000 vitapatikana na hivyo kuwatoa shaka kuwa wakazi wote zaidi ya 3000 waliohakikiwa kila mmoja atapata ardhi iliyopimwa huku wenye mashamba nao wakipata viwanja vitakavyobakia ili waweze kuviendeleza au kuviuza vikiwa na hati miliki.
DC Hapi ameongeza kuwa kazi ya upimaji wa ardhi katika eneo hilo inatarajiwa kuanza haraka na kumalizika ndani ya kipindi cha miezi mitatu chini ya kampuni ya Afro Map ambayo pande mbili zimeichagua kufanya kazi hiyo.
"Nawapa kampuni hii miezi mitatu tu, kazi ya upimaji iwe imekamilika eneo hili ili wananchi wangu waishi kwa amani wakijua serikali yao ipo kuwasaidia."
Alisema DC.
Mgogoro wa Nakasangwe ulianza mwaka 2004 na hivyo kudumu kwa miaka takribani 13 kipindi ambacho kilitawaliwa na chuki, uhasama na uadui mkubwa baina ya wenye mashamba na wananchi waliovamia mashamba hayo na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha katika mgogoro huo.
Wananch wote wanaounda pande mbili za mgogoro wamemshukuru DC Hapi na kushikana mikono kama ishara ya mwisho wa mgogoro huo na mwanzo mpya.
Imetolewa na
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
Wilaya ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.