Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe amepongeza Wakandarasi wa kampuni ya Estim pamoja na Wakala wa barabara vijijini na mjini (TARURA) kwa kazi kubwa waliyoifanya ya utekelezaji wa mradi wa matengenezo ya barabara ya Toure drive kwa kiwango cha lami iliyopo Masaki yenye urefu wa kilometa 3.5.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, DC Gondwe alisema ni jambo kubwa kuona mradi huu wa ujenzi wa barabara unaendelea vizuri kutokana na uchapakaji kazi wa wafanya kazi kwa weledi na umakini.
''Niwapongeze wakandarasi wa Estim kwa kushirikiana na TARURA, kwa kufikia hatua ya utekelezaji wa mradi huu asilimia 66 ni jambo kubwa na zuri, siku zote kazi tunapaswa kufanya kazi kwa vitendo na wala sio kwa maneno.
''Nimefurahi kuona katika mradi huu kuna njia ya watembea kwa miguu ambayo itawasaidia wananchi kuweza kutembea katika njia ambazo ni salama kwao," Alisema DC Gondwe.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuhusiana na njia za watembea kwa miguu kusiwekwe biashara ya aina yoyote ile kwani maeneo hayo ni kwa ajili ya watembea kwa miguu na wala sio kwa wafanyabiashara.
Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi. Stella Msofe kwa upande wake aliwataka wakandarasi kuendelea kufanya kazi vizuri kwa kuzingatia misingi inayotakiwa kufuatwa. "Niwapongeze Estim pamoja na TARURA kwa juhudi kubwa waliyoifanya, nina imani mradi huu utakamilika kwa wakati sahihi uliopangwa," alisema DAS Stella.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Peter, alisema mradi huo wenye urefu wa kilometa 3.5 ambao unahusisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ikiwa na mifereji ya pembeni pamoja na barabara ya watembea kwa miguu una gharimu shilingi za Kitanzania bilioni 5.6 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 66 ya ujenzi.
''Barabara itawasaidia wananchi kutalii kwa sababu ipo pembeni mwa bahari, lakini pia barabara za watembea kwa miguu itawasaidia wale ambao wanapenda kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao," Alisema Peter.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.