Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo ameiasa jamii kutojihusisha na tabia ya kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu kwakuwa na wao wana haki ya kupata haki zote kama ilivyo kwa watu wengine.
Mhe. Chongolo ametoa kauli hiyo leo wakati wa uzinduzi wa kamati ya watu wenye ulemavu uliofanyika Manispaa ya Kinondoni ambapo pamoja na mambo mengine amesema ipo dhana iliyojengeka ya kuwanyanyapaa watu hao na hivyo kueleza kuwa kufanya hivyo ni makosa na kusisitiza kuwa nilazima itendeke haki na usawa.
Amesisitiza kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kupewa nafasi mbalimbali na kusema kuwa wote wenye dhamana ya uongozi katika Halmashauri hiyo ni lazima kuangalia makundi hayo kwa upekee zaidi kwa kutenda haki na usawa.
Mhe. Chongolo amefafanua kuwa ili kufikia malengo hayo kila mmoja hakuna budi kushirikiana na kamati hiyo iliyoundwa kuweka miundombinu sawia itakayowezesha walemavu kuishi kwa kupata haki zao na usawa pamoja na kuepusha kunyanyapaliwa kama ilivyo kwa sasa.
“ Nawashukuru sana kwakunipa heshima hii ya kuzindua kamati hii ambayo inalenga kusimamia, kushughulikia ipasavyo kutetea haki na usawa wawatu wenye ulemavu” amesema Mhe. Chongolo.
Mhe. Chongolo hakusita kueleza changamoto mbalimbali zilizopo katika Halmashauri ya Kinondoni na kusema kuwa sio vijijini tu hata mijini wapo baadhi ya watu wanao wanyanyapaa walemavu kwakuwatenga, kuwaficha pamoja na kuwanyima fursa yakupatiwa huduma kama watu wengine.
“ Jamii imekuwa na taswira mbaya yakuona kwamba ulemavu ni changamoto iliyokuwa na madhara , na hivyo kujikita kunyanyapaa, kamati hii imepewa mamlaka, sasa nendeni mkajenge timu nzuri itakayoleta sura ya kubadilisha mtazamo uliopo hivi sasa na kuleta matunda na faida kwao.
Awali taarifa ya watu wenye ulemavu, ilieleza kuwa halmashauri inajumla ya kata 20 ambazo zinahudumia watu hao wapatao 1239 ambapo kati yao wanaume ni 724 na wanawake 515.
Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa kati ya watu hao wakubwa ni 973 huku watoto wakiwa 266 na kwamba huduma hizo zinatolewa kwakuzingatia sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, sheria namba 9 ya mwaka 2010 pamoja na mikataba mbalimbali inayohusu watu wenye ulemavu.
Ameeleza kuwa , Halmashauri imekuwa ikiviwezesha vyama vya watu wenye ulemavu kwa kuvipatia vifaa saidizi kulingana na aina ya ulemavu sambamba na kuwapatia misaada au kujikimu kwa walio na mazingira hatarishi.
Aidha ameeleza kuwa , Kinondoni imekuwa ikiwaunganisha na asasi za kiraia ili waweze kujipatia ujuzi , ajira na misaada ya kujikumu palipo na uhitaji pamoja na kuwawezesha maadhimisho ya watu wenye ulemavu yanayofanyika kila mwaka.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.