Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Godwin Gondwe, ametoa saa 24 kwa DAWASCO kupeleka maji kwenye Soko la Wamachinga la Cocacola, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Agizo hilo amelitoa leo wakati akipokea meza 300 za wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) zilizotolewa na Kampuni ya Cocacola jijini Dar es Salaam. Alisema, “Nimepokea ombi lenu, hivyo ninaagiza kuwa DAWASCO ndani ya masaa 24 kuanzia leo muwe mmepeleka maji kwenye soko hilo.”
Agizo hilo limefuatia ombi la Mwenyekiti wa wafanyabiajshara hao, Bw. Abdallah Mwakilima, aliyeomba kupatiwa huduma ya maji ili yaweze kutumika katika choo kilichojengwa na Manispaa ya Kinondoni. “Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, tunaomba utuzindulie choo chetu ambacho Manispaa imekijenga kwa gharama ya shilingi milioni 50. Tatizo lililopo ni kuwa choo hicho hakina maji,” alisema Mwakilima.
Kampuni ya Cocacola imetoa meza bure kwa wafanyabiashara hao ikiwa ni lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita za kuwapatia mazingira mazuri wafanyabiashara hao.
Aidha Bw. Mwakilima pamoja na kutoa shukrani kwa Manispaa ya Kinondoni na kwa Kampuni ya Cocacola, pia aliomba eneo hilo kuwekewa kivuli ili kuwakinga dhidi ya jua na mvua wafanyabiashara hao.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi Hanifa Suleiman Hamza, aliwataka wafanyabiashara hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali na Kampuni ya Cocacola.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mheshimiwa Songoro Mnyonge, alisema kuwa zoezi la kuwapatia vitendea kazi wafanyabiashara hao ni mwendelezo wa kampeni ya Safisha Pendezesha Dar es Salaam. “Wafanyabiashara mkikaa sehemu nzuri kwa kupangwa pia inasaidia kuisafisha na kuipendezesha Manispaa yetu ya Kinondoni,” alisema.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.