Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Stella Msofe amewataka wazazi/walezi kutoa ushirikiano katika kampeni ya utoaji chanjo ya matone ya polio kwa watoto iliyoanza Septemba mosi mpaka Septemba 4, 2022.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo katika Kituo cha afya cha Magomeni, Katibu Tawala huyo ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe amesema wazazi/walezi kutokumpatia mtoto chanjo ni kumkosesha haki muhimu ya kumlinda dhidi ya magonjwa ya kupooza.
Amesema kwamba matarajio ya Mkuu wa Wilaya ni kuona tunafikia malengo yetu ya kuwafikia watoto wote walio na umri chini ya miaka mitano wapatao 223,541 kwa muda wa siku nne za kampeni ambayo ni ya awamu ya tatu.
"Tutoe ushirikiano kwa wataalamu wa afya kwa kuwatoa watoto waweze kupata chanjo ya matone ya polio ili kuwakinga na ugonjwa wa kupooza (POLIO), na wala msiogope", Alisema Msofe.
Naye Mganga mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Dkt. Samwel Laizer ametoa tahadhari kwa wazazi/walezi kuhusu tukio lililotokea nchini Msumbiji la mtoto kupata ulemavu wa ghafla uliosababishwa na ugonjwa wa polio. "Wazazi zoezi hili ni la muhimu sana kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa ya kupooza, toeni watoto wapate chanjo"
Imeandaliwa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.