Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo ameliagiza Jeshi la Polisi Wilayani hapo kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuingia kwenye mito na kuchimba mchanga katika bonde la mto Salasala, bonde la mto Mbezi na bonde la mto Tegemeta.
Mhe. Chongolo ametoa agizo hilo leo wakati alipofanya ziara na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kushuhudia vitendo hivyo vikiendelea ikiwa ni takribani miezi miwili imepita tangu kuendesha zoezi la upandaji miti ya mianzi na magugu pamoja na kusitishwa kwa vibali vya uchimbaji wa mchanga vilivyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ruvu.
Amesema kuwa licha ya kutoa maelekezo pamoja na kusitishwa kwa vibali hivyo lakini bado wananchi wanaendelea kuchimba mchanga jambo ambalo amesema linahatarisha nyumba za makazi ya watu na hivyo kulisisitizia jeshi hilo kuwachukulia hatua wananchi hao ambao wanajihusisha na shuguli hizo.
“Tulishazuia hii mito isichimbwe mchanga, tumepita mto Salasala, Mbezi kule kwenye daraja la Malechela, pamoja na huku juu mpakani mwa eneo la jeshi la Lugalo, bado vitendo hivi vinaendelea nasisitiza naninaagiza jeshi la polisi kwenye Wilaya ya Mabwepande na Kawe ambayo ndio inahusika, niliagiza na leo narudia kwa mara ya pili hatutakuwa na msamaha kwenye jambo hili.
Amefafanua kuwa “mtu yeyote ambaye ataonekana analea vitendo vya uharibifu huu wa mazingira, tukimkuta na kumkamata tutamchukulia hatua kali za kisheria kwasababu jukumu letu sisi viongozi ni kusimamia na kuilinda sheria.
Mhe. Chongolo amesisitiza kuwa“ Hatuko hapa kuwaonea watu, wala kuwaacha wananchi waharibikiwe na nyumba zao kwasababu ya maslahi na uroho wa watu wachache, kufanya hivi ni kuhujumu maslahi ya nchi hatuwezi kuendelea kuwaacha watu wanamna hii kwa hiyo nilazima tuchukue hatua kwa kila tutakaye mbaini anafanya shughuli hii.
Aidha Mhe. Chongolo amesema kuwa baada ya ziara hiyo ataunda timu ya kufuatilia mwenendo wa watu hao kwa kuwa alishatoa maagizo ya kuwashugulikia wote wanaohusika na kufanya shuguli za kuchimba mchanga kwenye mito hiyo.
Mapema mwaka huu, Mhe. Chongolo alisitisha vibali vya uchimbaji mchanga vilivyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ruvu kutokana na kuleta madhara ya uharibifu wa mito na kusababisha athari kwenye makazi ya watu katika Halmashauri hiyo.
Vibali vilivyositishwa ni vile vilivyotolewa kufanya shughuli hizo katika Bonde la mto Salasala, Mto mbezi, Ndumbwi, Nyakasangwe, na kusema kuwa mito hiyo inapita katikati ya makazi ya watu na kwamba baada ya kufanyika marekebisho utawekwa utaratibu upya wa kufanya shughuli hizo.
Imeandaliwa na Kitengo Cha Habari na uhusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.