Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, imezindua Bodi ya Zabuni yenye wajumbe saba, inayotarajia kufanya kazi yake kwa kipindi cha miaka mitatu, kwa ajili ya kushughulikia maswala ya manunuzi kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya mwaka 2011, pamoja na kanuni zake.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa na kuhudhuriwa na wajumbe wa PMU wa Manispaa hiyo, pamoja na watumishi wengine.
Akizindua bodi hiyo,kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Ndg Maximilian Tabonwa, ambaye pia ni Mwekahazina wa Manispaa hiyo amesema uzinduzi huo ni kwa mujibu wa vifungu vya 36(1)(a) na (b) vya sheria ya manunuzi ya Umma namba 7 ya mwaka 2011, pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 vinavyompa Afisa Masuuli /Mkurugenzi mamlaka ya kuanzisha bodi ya zabuni katika taasisi na kuteua wajumbe wa bodi ya Zabuni.
Amesema uteuzi wa wajumbe umefanyika baada ya mchakato wake kisheria kukamilika na kupitishwa kwenye kamati ya kudumu ya Fedha na Uongozi kwa baraka zao ambapo watatakiwa kuanza kazi rasmi baada ya kutangazwa kwao.
Ameyataja majina ya wajumbe hao kuwa ni Dr. Patricia Henjewele, ambaye ni mwenyekiti wa bodi, Dr. Festo Dugange, Ndg Maduhu Kazi, Injinia Emanuel Mwampashi, Ndg Kiduma Mageni, Ndg Hussein Ugulumu na Ndg Raphael Wariana ambaye ni katibu wa bodi.
Aidha ameainisha majukumu yao kuwa ni kijadili mapendekezo yaliyoletwa na kitengo cha manunuzi, kufanya mapitio ya maombi yote ya nyongeza, agenda au marekebisho ya mikataba inayoendelea, Kuidhinisha zabuni na mikataba, kuidhinisha manunuzi na uuzaji wa njia ya zabuni na kuhakikisha mifano mizuri na taratibu za manunuzi na uuzaji kwa njia ya zabuni inafuatwa na kuzingatiwa.
Pia ameainisha madaraka ya bodi hiyo kuwa ni kuomba ushauri wa kitalam au kitaaluma kutoka kwenye mamlaka yeyote, kuchunguza nyaraka au kumbukumbu na kuchukua nakala au kiziduo pamoja kufanya jambo lolote kama itakavyoona inafaa kufikia malengo yake.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa bodi hiyo Dr. Patricia Henjewele ambaye pia ni Afisa Mifugo wa Manispaa ameahidi kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia misingi ya kazi itakayoleta tija kwa Halmashauri yetu.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.