Bodi ya Afya chini ya Sheria ya Serikali ya Mitaa (Mamlaka ya Wilaya), Sura na 287, Mamlaka ya Miji sura na 288, pamoja na mwongozo wa uundaji na uendeshaji wa Bodi za Afya za Halmashauri na kamati zake wa mwaka 2013, itakayofanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya mwenyekiti wake Ndg Bernard lwehabura Manispaa ya Kinondoni imezinduliwa leo.
Akizindua Bodi hiyo leo yenye wajumbe 13, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Alli Hapi amesema uundwaji wake umezingatia sheria, taratibu na vigezo vyote, hivyo imepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, katika misingi ya ushirikishwaji na utatuzi wa changamoto, ambayo ndiyo njia sahihi itakayoleta maendeleo kwenye sekta ya Afya.
"Mnayokazi kubwa mbele yenu, ya kuvaa viatu ambavyo wenzenu viliwaenea sawasawa, tunategemea dhamana mliyopewa, malengo mliyojiwekea kuwatumikia wananchi yanatimia "Amesisitiza Hapi.
Awali akisoma taarifa ya bodi kwa Mkuu huyo wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dr Festo Dugange amesema uundwaji wa Bodi hii umezingatia mwongozo wa uundaji wa bodi wa mwaka 2013, na kwamba inayo wajibu wa kusimamia shughuli zote za Afya katika Manispaa ya Kinondoni.
Aidha ameyataja majukumu mengine ya Bodi kuwa ni kuandaa mipango shirikishi ya Afya inayotilia mkazo mahitaji yote, kuhakikisha vituo vya afya, hospital, na zahanati vinatekeleza shughuli za Afya, kuhakikisha uwepo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika maeneo hayo unazingatiwa, kuwa tayari kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na upatikanaji wa watumishi wa afya wenye taaluma hizo.
Nyingine ni watoa huduma za Afya kuzingatia sheria, kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa kuzingatia sheria na maadili, kuhakikisha takwimu zinakusanywa na kuchambuliwa, na kujumuisha na kuchambua taarifa za utekelezaji wa bodi za robo.
Uzinduzi huo ulienda sambasamba na ukabidhiwaji wa miongozo ya utendaji kwa wajumbe, ambapo Bodi itapokea mpango shirikishi wa Afya unaojumuisha mipango ya Afya ya vituo vya huduma na taarifa za utekelezaji wa fedha za kila robo mwaka na za mwaka zinazohusu mipango na hali ya Afya kutoka timu ya uendeshaji huduma za Afya ya Halmashauri.
Imetolewa na
Kitengo cha habari na Uhusiano.
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.