SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo, imetenga kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 950 kwa ajili ya uboreshaji kilimo na miundombinu ya umwagiliaji nchini.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, ameyabainisha hayo wakati akizindua maonesho ya Nane Nane Mkoani Morogoro Agosti 01, 2023.
Mheshimiwa Pinda alisema kuwa, "Serikali imetenga bajeti ya Shilingi za Kitanzania bilioni 950 kwenye kilimo, miundombinu ya umwagiliaji, ubora wa mbegu, upatikanaji wa mbolea, upimaji wa afya ya udongo na kuongeza matrekta kwa ajili ya kilimo".
Aidha, ameitaka Kanda ya Mashariki kutoa kipaumbele kwa wafugaji, wavuvi na wakulima ili kufanikiwa katika sekta hizo. Alisisitiza kuwa, "tutumie fursa ya nguvu kazi iliyopo kuweza kufanikiwa kwenye kila sekta na kujipanga kwa ajili kujitosheleza kwa chakula".
Mheshimiwa Pinda pia amezitaka taasisi za kifedha nchini kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake na vijana katika kukuza kilimo nchini.
Maonesho hayo yanayoendelea mkoani hapa yakiwa na kauli mbiu "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula" yanashirikisha Taasisi mbalimbali ikiwemo Manispaa ya Kinondoni.
Manispaa ya Kinondoni inashiriki katika kutoa elimu kuhusiana na masuala ya Ushirika; Kilimo, Ufugaji na Uvuvi haswa kwa wanaoishi mijini.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini: Manispaa ya Kinondoni
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.