Pongezi hizo zimetolewa na Mst. Meya wa Manispaa hiyo Mh. Benjamini Sitta wakati wa kikao cha Baraza la madiwani robo ya tatu ya mwaka kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa.
Meya Sitta amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wake, yeye pamoja na Baraza lake wameshuhudia uzalendo na umahiri wa watendaji pamoja na viongozi wa Halmashauri katika kusimamia rasilimali za Serikali kwa kiwango cha ubora unaoridhisha hasa katika suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Halmashauri hiyo.
“Niseme tu kwamba Kinondoni imepata Mkurugenzi bora na mzalendo, amekuwa kiongozi hodari katika kuhakikisha vipaumbele vya Halmashauri vimetekelezwa, hasa vile vinavyomgusa mwananchi moja kwa moja vimepewa kipaumbele cha kutosha na vimekamilika kwa usahihi na ubora uliokusudiwa” Amefafanua Meya Sitta.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mipangomiji na Mazingira alipokuwa akichangia mada katika kikao hicho amesema kuwa, Kinondoni imekuwa na mafanikio makubwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, Afya, Miundombinu Masoko na Mazingira ikiwa ni pamoja na utengaji wa asilimia kumi kwa ajili ya mikopo ya vijana, wazee na walemavu kufikia walengwa kwa wakati.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni Stendi ya Kisasa ya daladala ya Mwenge, Ofisi ya kisasa ya Manispaa, uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, Soko la kisasa Magomeni, Tandale ambapo yote inatekelezwa na mapato ya ndani.
Akitoa shukrani katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg. Aron Kagurumjuli ameeleza kuwa, mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo umetokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya ofisi yake na Meya pamoja na watendaji, kwani kila mmoja amekuwa akitimiza majukumu yake pasipokuwa na migongano, iliyopelekea ufanisi katika nyanja zote za Elimu Sekondari, Afya, Masoko Miundombinu ya barabara pamoja na Mazingira.
“Tangu tumeingia kwenye utawala huu, nikiwa na Meya Sitta hatujawahi kuwa na migogoro, watendaji wamekuwa na muda mwingi wa kufikiria mambo makubwa ya maendeleo jambo ambalo limetufikisha tulipo hapa, kwenye mafanikio makubwa nandio mana leo tunapongezana hapa”, Ameeleza Kagurumjuli.
Katika hatua nyingine baraza hizo limepitisha taarifa za kamati mbalimbali ambazo ni kamati ya Fedha na uongozi, Huduma za Uchumi, Kamati ya kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Maadili pamoja na kamati ya mipango miji na mazingira.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.