Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, katika Mkutano wake maalumu wa Baraza leo Alhamisi, tarehe 23 Januari 2020, limejadili na kuidhinisha kwa kauli moja bajeti yake ya Tshs 170, 918,524,100/= kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo Tshs.42,951,312, 000/= ni za Mapato ya ndani ya Manispaa na Tshs. 127,967,212,100/= ni Mapato ya Ruzuku kutoka Serikali kuu zikijumuisha Tshs. 57,018,968,680/= kwa ajili ya mishahara,Tshs.1,689,501,000/= za matumizi mengineyo na Tshs. 69,258,742,520, /= za miradi ya maendeleo.
Kiasi cha ,Tshs. 42,951,312,000/= kilichotengwa na Manispaa ya Kinondoni kutokana na makusanyo ya vyanzo vya ndani vya, Manispaa kinajumuisha Tshs.883,467,270/=, kwa ajili ya mishahara ,Tshs. 21,353,714,130,000/= kwa ajili ya matumizi mengineyo na Tshs. 20,714,130,000/= kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Azungumza wakati wa kupitisha Bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mh Benjamin Sitta amebainisha kuwa ili kuboresha maisha ya wakazi wa Kinondoni, Manispaa imeandaa mpango wa mwaka 2020/2021 na mpango wa muda wa kati 2020/2021 – 2022/2023 unaolenga kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kufikia maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi,na kimazingira kwa wananchi wake.
Meya Sitta ametanabaisha kuwa Ili kutekeleza dhana nzima ya ugatuaji wa madaraka , mpango huo umeshirikisha jamii katika mpango shirikishi kuanzia ngazi ya Mtaa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji halisi ya Wananchi katika maeneo yao na kujielekeza katika kutoa kipaumbele maeneo yanayoweza kutoa matokeo ya haraka yatakayosaidia ukuaji wa uchumi kwa haraka na kwa kipindi kifupi.
Ameyataja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuwekeza katika miradi mikubwa ya Kimkakati, kuboresha miundombinu ya Afya, na Elimu,kuboresha hifadhi ya mazingira na ukusanyaji wa taka, kuimarisha ushirikishaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na uboreshaji wa mazingira ya wafanyabiashara wadogowadogo kwa kuwajengea masoko katika maeneo mbalimbali.
Ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, Mstahiki Meya amewataka viongozi na watendaji wote kusimamia uimarishaji wa mahusiano mazuri kati ya Serikali ,Mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine, kujenga uwezo na ujuzi kwa watumishi katika utoaji wa huduma, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na uwazi sambamba na kujenga uwezo kwa viongozi wakiwemo waheshimiwa madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa katika kusimamia shughuli za Wananchi.
Aidha Mstahiki Meya amewashukuru wadau wote waliofanikisha bajeti hiyo zikiwemo kamati zote za kudumu za Manispaa, Serikali kuu iliyotenga kiasi kikubwa cha fedha kugharamia Miradi mikubwa ya kimkakati ya ujenzi wa soko la Tandale, Soko la Magomeni uboreshaji wa Fukwe za Cocobeach na miradi mingine ya sekta mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Manispaa ya Kinondoni kwa Fedha kutoka Serikali kuu.
Miradi iliyotengewa fedha kwa Mapato ya ndani ya Manispaa katika mwaka wa fedha 2020/2021 ni pamoja na ukamilishaji wa kituo cha kisasa cha daladala Mwenge kwa milioni 500, ukamilishaji ujenzi wa uwanja wa mpira Mwenge kwa milioni 500, ujenzi wa standi ya kisasa ya daladala na soko Tegeta nyuki kwa bilioni 3.5, ujenzi wa kituo cha kisasa cha daladala Bunju B kwa milioni 600,ujenzi wa maabara, famasia, rediolojia, na ununuzi wa gari la kubeba wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya Mabwepande kwa bilioni 1 na ujenzi wa incinerator kubwa kwa ajili ya kuchoma taka za vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa billion 1.5.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.