Mkoa wa Dar es Salaam ni muhimu sana katika uchumi wa Tanzania. Unapatikana katika pwani ya Bahari ya Hindi na una Bandari kubwa katika Afrika mashariki unaoufanya mkoa huu kuwa mashuhuri sana kiuchumu. Una miundombinu ya uhakika ambayo ni barabara nzuri za lami, hoteli zenye hadhi ya kuanzia nyota 1 hadi 5 na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ujulikanao kama (Mwalimu Nyerere International Airport). Uwepo wa Bandari kubwa na ya kisasa unaufanya Mkoa uweze kufikika kirahisi kwa kupitia Baharini na Nchikavu kutoka katika kila pembe ya Dunia na kuwa kiungo muhimu katika Sekta ya Utalii.
Mkoa wa Dar es Salaam hauko nyuma katika Sekta ya utalii. Mkoa huu una vivutio vingi ambavyo ni muhimu katika kuvutia watalii. Vivutio vya asili vilivyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ni Bahari yenye fukwe nzuri, Misitu ya Mikoko na Miyombo, Visiwa, Matumbawe na hifadhi ya wanyama Dar es Salaam zoo.
Dar es Salaam ina uoto wa asili wa aina mbili ambao ni Misitu ya Mikoko yenye ukubwa wa hekta 2,760 na Miyombo yenye ukubwa wa hekta 1,380. Misitu ya Mikoko inapatikana katika mwabao wa Bahari ya Hindi na Misitu ya Miyombo inapakika katika maeneo ya uwanda wa juu. Misitu hii imehifadhiwa kwa ajili ya makazi na mazalia ya viumbe wa baharini na nchi kavu na ni kivutio kizuri cha utalii katika mkoa wetu.
Uwepo wa Bahari ya Hindi katika Mkoa huu ni kivutio kizuri sana cha utalii kwa kutoa muonekano unaovutia na kuleta upepo mzuri. Bahari inaweza kutumika kwa kufanya mashindano ya kuendesha boti pamoja na kuogelea. Bahari vilevile ni hifadhi ya samaki wengi wanaovutia. Ufukwe mzuri wa Koko wenye eneo kubwa la kupumzika ni kivutio kizuri cha utalii kwa wenyeji na wageni
Mkoa vilevile una visiwa vikubwa vitatu vilivyo umbali kidogo kutoka katika ufukwe wa Bahari. Visiwa hivyo ni Mbudya, Bongoyo na Pangavini. Visiwa hivi vina misitu mikubwa ya asili inayopendesha mazingira na ni makazi ya viumbe wa nchi kavu kama vile ndege na nyoka. Vimezungukwa na miamba ya matumbawe (coral reefs) ya rangi mbalimbali na ni mazalia ya samaki.
Mkoa huu una vivutio vingi vya kale ambavyo ni mabaki ya tokea Utawala wa Mwarabu, Mjerumani na Muingereza pamoja na mabaki ya zana na watu wa kale. Mabaki haya yanaonekana kama alama zilizopo ardhini na kwenye majengo.
Ushirikiano na Miji mingine ya Utalii Duniani ni jambo muhimu sana, tunaweza kuibadilisha Dar es Salaam kuwa Jiji kuu la Utalii Duniani na kuliongezea Taifa kipato. Si hivyo tu bali uchumi wa watu utabadilika na kupunguza umasikini. Kwa kuzingatia kwamba Serikali yetu inasisitiza mabadiliko katika kuboresha uchumi wa viwanda ili kuondoa umasikini na kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
2 Barabara ya Morogoro, 14883 Dar es Salaam
Anuani ya Posta: S.L.P 31902
Simu ya mezani: +255222170173
Simu ya mkononi: +255733241052
Barua pepe: md@kinondonimc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Haki Zote Zimehifadhiwa.